06/06/2026
NENO LA SIKU
Na, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira – Kanisa la Efatha
TAREHE: 06/06/2026
SOMO: MTAFUTE MUNGU KWA BIDII
Mungu wetu hufurahia watu wenye unyenyekevu na moyo wa kuzingatia. Watu wengi wamepoteza nafasi zao si kwa sababu hawakuwa na uwezo, bali kwa sababu ya uzembe na kutokuzingatia.
Esau alipoteza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa uzembe. Mfalme Sauli naye alipoteza ufalme kwa kushindwa kufuata maelekezo ya Mungu. Haya yanatufundisha kuwa uzembe unaweza kugharimu hatima ya mtu.
Heri yako unayezingatia mambo ya Mungu na kuthamini uwepo wake. Heri yako unayejitahidi kuwa ibadani na kumtafuta Mungu hata pale hali ya mwili inapokuwa ngumu. Biblia inasema katika Zaburi 122:1 “Nalifurahi waliponiambia, twende nyumbani mwa Bwana.”
Wapo wanaohitaji kusukumwa ili waende kanisani au kumtafuta Mungu. Lakini wapo ambao hawahitaji kukumbushwa, kwa sababu shauku ya Kristo imo ndani yao. Jenga tabia ya kumtafuta Mungu kwa hiari, kwa bidii na kwa moyo wote.