18/05/2026
Mohsen Rezaei, ambaye ni mwanachama wa Baraza la Ushauri la Maslahi ya Taifa la Iran na k**anda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ameionya Marekani kusitisha kile alichokiita mzingiro wa kijeshi wa majini dhidi ya bandari za Iran.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa ya Iran, Rezaei alisema kuwa jeshi la Iran liko tayari kwa mapambano zaidi iwapo Marekani itaendelea na hatua hiyo.
Aliongeza kuwa Bahari ya Oman inaweza kuwa “kaburi” la majeshi ya Marekani endapo mvutano utaongezeka.
Rezaei alieleza kuwa hatua ya Marekani kuzuia shughuli za majini za Iran ni “tendo la vita” na kwamba Iran ina haki ya kujibu kwa kujilinda.
Aidha, alisema kuendelea kwa vikwazo hivyo kutasababisha madhara makubwa kwa mataifa mengi duniani, hasa kupitia usumbufu wa biashara za kimataifa na soko la nishati katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, licha ya matamshi hayo makali, Rezaei alisema bado kuna juhudi za kidiplomasia zinazoendelea ili kumaliza mzozo huo.
Alisisitiza kuwa sasa ni jukumu la Marekani kuonyesha nia ya kweli ya kutafuta suluhisho la amani. Kwa mujibu wake, vikosi vya Iran viko tayari kijeshi, lakini milango ya diplomasia bado iko wazi.