14/06/2026
UZIO UMEANGUSHWA, MWALI KATOKA NJE
Hayawi hayawi sasa yamekuwa na mwanzo wa ngoma ni lele, hatimaye Faru weupe walioingizwa nchini kutoka Afrika kusini na kuhifadhiwa kwenye uzio maalum tarehe 13 Juni, 2026 wameachiwa huru kujivinjari katika viunga vya kreta ya Ngorongoro ili kuungana na wenyeji wao Faru Weusi katika Kasoko ya Ngorongoro.
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande ameongoza timu ya wizara,menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wa AndBeyond kuwaachia faru hao ambao idadi yao ni 17.
Faru hao wameletwa nchini na kupandikizwa Kreta ya Ngorongoro mahsusi kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, utafiti na elimu kutokana na nchi ya Tanzania kuonekana kuwa ni sehemu salama kiulinzi, Kiuhifadhi na mazingira mujaarabu kwa spishi ya Faru hao ambao wapo kwenye kundi la Wanyama waliopo hatarini kutoweka.
Mhe. Chande ameipongeza kampuni ya AndBeyond kutokanana na kutambua umuhimu mkubwa wa Uhifadhi na utafiti katika nchi mbalimbali duniani huku akipongeza uongozi na Askari wa Ngorongoro kwa kuwa mstari wa mbele kuwalea, kuwatunza, kuwahifadhi na kulinda Faru Weupe ambao walitoweka katika Nchi yetu kwa takribani miaka 300 iliyopita.
Akizungumza katika hafla hiyo mkurugenzi wa wanyamapori wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Alexander Lobora amesema mchakato wa kuwaleta wanyama hao nchini utatoa fursa kwa Wadau wa utafiti na mafunzo kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Abdul-Razaq Badru amesema Ngorongoro ni sehemu salama kwa uhifadhi,utafiti na mafunzo ambapo ametoa wito kwa wadau kuendelea kuitumia mamlaka hiyo katika shughuli hizo.
Faru hao weupe 17 kuachiwa huru na kutamba ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ni Mwanzo wa Safari ya awamu ya pili kuleta Faru Weupe 18 kutoka Afrika Kusini kwa siku zijazo.